Habari Forums
Would you like to react to this message? Create an account in a few clicks or log in to continue.
Search
 
 

Display results as :
 


Rechercher Advanced Search

Keywords

mwanamke  Jinsi  

Latest topics
» MATOKEO YA AWALI UCHAGUZI MKUU 2015
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySun Oct 25, 2015 7:59 pm by Admin

» Upinzani Tanzania wazindua kampeni
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySat Aug 29, 2015 8:11 pm by Admin

» Joke Of the Day
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySun Jun 07, 2015 12:53 pm by Admin

» Tatizo sugu LA Ajira
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySat Jun 06, 2015 7:29 pm by Admin

» Joke Of the Day
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySat Jun 06, 2015 7:28 pm by Admin

» Joke Of the Day
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySat Jun 06, 2015 7:26 pm by Admin

» * MAFURIKO MAKUBWA YATOKEA MWANZA....
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptySat Jun 06, 2015 12:35 pm by Admin

» Lakini ungeweza Kama ungetaka
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptyWed Jun 03, 2015 1:03 pm by Admin

» Fun fact teehe
Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha EmptyWed Jun 03, 2015 8:21 am by Admin

May 2024
MonTueWedThuFriSatSun
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
2728293031  

Calendar Calendar


Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha

Go down

Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha Empty Hali tete Chuo Kikuu cha Mt Joseph Arusha

Post by Admin Wed Mar 11, 2015 9:04 am

MGOGORO ulioibuka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Arusha baina uongozi wa chuo na wanafunzi umechukua sura mpya kwa hatua ya mmoja wa wahadhiri wa chuo hicho kutoka nchini India kujitokeza hadharani na kuanika “maovu” yanayofanywa na uongozi.
Mhadhiri huyo, Irimia Edava, alifika katika ofisi za Raia Mwema mjini Arusha mwishoni mwa wiki na akatoa tuhuma nzito dhidi ya uongozi wa chuo hicho ambacho kina matawi pia Jijini Dar es Salaam, Peramiho mkoani Ruvuma na Makambako mkoani Njombe.
Katika toleo lake namba 394 gazeti hili liliripoti kuwa uongozi wa chuo hicho unatuhumiwa kuwanyanyasa wanafunzi wanasoma chuoni hapo kwa kuwanyima haki mbalimbali za msingi na mwanafunzi huku mwanafunzi mmoja akiachishwa chuo kwa sababu ya kuumwa ugonjwa wa kisukari.
Wanafunzi pia waliandika barua ya malalamiko kwa Waziri Elimu na Ufundi Stadi Dk. Shukuru Kawambwa, wakituhumu kuwa chuo hicho kinafundisha mitaala ya sayansi ya nchini India jambo ambalo hata TCU walibaini katika uchunguzi walioufanya.
Mhadhiri huyo alieleza kuwa aliajiriwa na chuo hicho chenye matawi katika nchi kadhaa za Afrika Juni mwaka 2014 na kuanza kazi nchini Zambia katika chuo cha Mtakatifu Eugene kama Mhadhiri Msaidizi wa somo la Kemia.
“Nikiwa nchini India tulikubaliana na uongozi wa chuo kuwa nakuja Afrika kufanya kazi ya kuwa Mhadhiri Msaidizi, na tulisainiana mkataba wa awali wa ajira lakini nilipofika Afrika nilibadilishiwa kibao kuwa ajira yangu ni ya kujitolea (voluntary) kinyume kabisa na makubaliano ya awali,” alieleza.
Mhadhiri huyo anathibitisha madai yake kwa kuonyesha barua yenye kumbukumbu namba DIR/EST/01124/667 iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Shughuli za Kimataifa wa mtandao wa chuo hicho Dk.T.X Annanth.
Katika barua hiyo ya Septemba 17 mwaka jana Mkurugenzi huyo anamwandikia barua Mhadhiri huyo na kumweleza kuwa atalipwa mshahara wa fedha za Kitanzania shilingi 780,000 kwa mwezi kama Mhadhiri anayejitolea tofauti na makubaliano ya awali waliyoafikiana nchini India.
‘Tulikuwa kama waalimu 30 hivi tuliokuja Afrika. Na wote walitufanyia hivyo na kibaya zaidi walichukua hati zetu zote za kusafiria pamoja na vyeti vyetu vya kitaaluma ambavyo wanavishikilia hadi hivi tunavyozungumza jambo ambalo kwa kweli ni kinyume cha sheria za nchi yoyote iliyostaarabika,” alisema.
Alidai kuwa kwa muda huo wote walikuwa wanaishi nchini kwa kutumia vibali ya kutembelea (visiting visa) huku wakiendelea kufanya kazi ambapo walilazimishwa kufanya kazi kuanzia saa 1.30 za asubuhi hadi saa 12.30 za jioni bila ya kupumzika kinyume kabisa cha sheria za kazi za kimataifa na Tanzania.
“Hata sasa wahadhiri karibu wote wanaishi kwa visa ya kutembelea lakini wanafanya kazi kinyume cha sheria za Tanzania kuhusu wafanyakazi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini ambao wanatakiwa kuwa na vibali vya kufanyia kazi, ” alidai.
“Baada ya kuona mazingira ya kazi ni magumu mimi pamoja na wenzangu tuliomba kujiuzulu na kuacha kazi kwa kuandika notisi ya miezi mitatu lakini uongozi wa chuo ulitaka tulipe fidia ya kati ya dola za Kimarekani 550-750, tulipojaribu kuhoji hawakuwa na majibu lakini waliendelea kudai tu na waliendelea kushikilia vyeti vyetu,” aliongeza.
Mhadhiri huyo aliongeza: “ Inasikitisha sana jinsi taasisi hii inavyotumia mwamvuli wa dini na jina la Mwenyezi Mungu vibaya kukandamiza haki za watu wengine pamoja na kuidanganya serikali kwa kukwepa kodi na tozo nyingine kwa kigezo kuwa ni taasisi ya dini ambayo imejikita katika kutoa huduma ya elimu kwa vijana masikini katika Bara la Afrika.
“Wahadhiri tunashangazwa na mamlaka za serikali ya Tanzania kukipa hadhi chuo hiki kuwa chuo kikuu. Chuo hakina vigezo hata kidogo kuwa taasisi ya elimu ya juu. Hivyo tunaungana na wanafunzi kuwa mabadiliko yanahitajika na tunaomba serikali kuangalia upya aidha chuo kifungwe au uongozi ulazimishwe kufanya marekebisho ya kweli.
“Chuo kina miundombinu mibovu kuanzia madarasa ambayo awali yalikuwa ni majengo ya kiwanda cha Wachina cha kutengeneza samani za nyumbani. Sasa maghala yamegeuzwa kuwa vyumba vya kufundishia. Hakuna hewa. Maabara haina vifaa vyovyote. Wanafunzi wanafundishwa nadharia tu. Haya si mazingira ya kutolea elimu ya juu.”
Alisema wanatoa wito kwa serikali na taasisi zinazohusika kuwasadia wahadhiri hao pamoja na wanafunzi ambao wamekuwa wanalalamikia masuala mabalimbali ya kitaaluma katika chuo hicho.
Wanafunzi wazidi kulalamikia TCU
Katika hatua nyingine wanafunzi wa chuo hicho wameendelea kulalamikia uongozi wa chuo hicho pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa kushindwa kutatua matatizo ya msingi chuoni hapo na badala yake kuendeleza vitisho dhidi ya wanafunzi.
Malalamiko hayo yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya TCU kumtuma mmoja wa maofisa wake Dk. A. Maronga ambaye wiki iliyopita alifanya vikao vya uongozi wa chuo na viongozi wa wanafunzi.
Katika waraka walioutoa kwa vyombo vya habari baada ya mikutano hiyo wanafunzi hao wanaelekeza lawama zao kwa ofisa huyo wa TCU kwa kushindwa na kukataa kukutana na wanafunzi wote badala yake akatumia muda mwingi kuusilikiliza uongozi wa chuo.
“Ujio wa kiongozi huyo wa TCU haukutatua kabisa matatizo sugu. Na badala yake tunaona umeongeza matatizo kwa majibu yake ya kibabaishaji na yenye utata mkubwa kwa sababu alikataa kupokea muhutasari wenye malalamiko ya wanafunzi,” walieleza wanafunzi hao.
“Ni vigumu sana kwa mtu yoyote kuweza kukumbuka maelezo yote yaliyozungumzwa kwa mdomo. Ofisa TCU hakutaka kuchukua muhutasari wa malalamiko ya wanafunzi alitaka tutume kwa njia ya posta hatua ambayo imetushangaza,” waliongeza.
“Kwa kila swali aliloulizwa na viongozi wa wanafunzi alijibu kisiasa, na kutumia ubabe kupunguza ukali na uhalisia wa tatizo hali iliyowafanya wanafunzi kushindwa kufikisha mawazo yetu kwa uhuru,” wanasema.
Wanafunzi hao wanadai kuwa miongoni mwa mambo ya msingi ambayo ofisa huyo wa TCU hakutaka kuyazungumzia ni pamoja na hatma ya wanafunzi walioachishwa masomo, waliozuiliwa kufanya mitihani kwa kuonewa.
“Hakuna kilichozungumzwa kuhusu wahadhiri wa Kihindi wasio na vigezo vya kufundisha chuo kikuu hasa kwa taaluma nyeti kama ya sayansi. Chuo hakina mhadhiri hata moja mwenye kiwango cha elimu ya profesa au phd. Wengi wana shahada ya uzamili na ni wa muda (part time).
“ TCU imeshindwa kutatua au kuwaunganisha wanafunzi na utawala. Kuna uhusama mkubwa. Ni jambo la hatari zaidi kwa wanafunzi ambao wazazi na walezi wao ni Watanzania wa kawaida waliolipa ada na mahitaji mengine kwa kujinyima ili watoto wao wasome wapate elimu,”walieleza.
Wanafunzi hao wanaiomba serikali ihamasihe utawala wa chuo kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ili wanafunzi waendelee na masomo, wanafunzi waliofukuzwa, kusimamishwa masomo kinyume na sheria warudishwe na pia chuo hicho kifuate mifumo ya vyuo vingine vya elimu ya juu.
Juhudi za Raia Mwema kuwapata viongozi wa chuo hicho hazikuweza kufanikiwa kutokana na urasimu. Mmoja wa viongozi wa juu wa chuo hicho aliyetajwa kwa jina la Sista Ramona (Mtawa wa Kanisa Katoliki) kama msemaji wa chuo simu yake ilipokelewa na alijieleza kuwa ni mfanyakazi wa ofisi.
“Sista hawezi kuzungumza na wewe mpaka unieleze mimi unamhitaji kwa ajili ya nini, ” alieleza mtumishi huyo.
Hata pale alipoelezwa kuwa ni mwandishi wa habari mtumishi huyo alijibu kwa mkato: “Mwandishi wa habari unataka nini? Nieleze kwanza shida halafu ndiyo nimweleze Sista,” alisema na kukata simu.
Kwa upande wake ofisa wa TCU Dk. Maronga hakuweza kupatikana.
Wiki iliyopita katika mazungumzo yake na Raia Mwema Katibu mtendaji wa TCU Profesa Yunus Mgaya alithibitisha kuwa ni kweli walipokea malalamiko ya wanafunzi hao na kuunda timu ya wataalamu iliyoongozwa na Profesa Kitila Mkumbo ambao waligundua kuwa na mapungufu makubwa katika chuo hicho.
Alisema timu hiyo ya wataalamu iligundua kuwa ni kweli mitaala iliyokuwa inatumika ilikuwa haikidhi mahitaji ya kitaaluma nchini Tanzania, na walishauriwa waibadilishe haraka mitaala hiyo.
“Uongozi wa chuo ulikiri mapungufu hayo na walikubali kuwa watarekebishe wakati wanafunzi wakiendelea masomo yao na tayari hilo limeshafanyika”aliongeza.
Profesa Mgaya aliongeza:”Kwa sasa matatizo yaliyopo yanaweza kurekebishika tofauti na matatizo yaliyowahi kutokea vyuo vingine kwa mfano kama yale ya chuo kikuu cha IMMTU”.
Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph kipo eneo la Kisongo nje kidogo ya mji wa Arusha na kinatoa shahada ya Elimu katika masomo ya Sayansi ya Fizikia, Kemia, Baolojia na Hesabu.

Admin
Admin

Posts : 54
Join date : 09/03/2015

https://habariforums.forumotion.com

Back to top Go down

Back to top


 
Permissions in this forum:
You cannot reply to topics in this forum